
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), limeikabidhi Serikali ya Tanzania dozi Mil. 3.9 za chanjo ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo kwenye hafla iliyofanyika, wakati wa Ufunguzi wa Warsha inayohusu Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la Afya ya wanyama Jijini Arusha.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa chanjo hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe amelishukuru Shirika hilo kwa msaada huo ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono mipango ya Serikali kupitia Wizara yake kwa mwaka huu wa fedha, ambapo imetenga takribani Shilingi Bil.28 kwa ajili ya kuendesha zoezi la chanjo ya mifugo nchi nzima.
Prof.Shemdoe ametoa rai kwa Mashirika mengine ya kimataifa na wadau wa Sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika eneo la uboreshaji wa afya ya wanyama ambapo amewaomba FAO kuongeza dozi nyingine za chanjo ili kukidhi idadi ya wanyama waliopo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa FAO Bi.Stela Kiambi ambaye ndiye aliyekabidhi chanjo hizo amesema kuwa Shirika lake linatambua kuwa afya bora ya wanyama inachangia afya bora ya binadamu hivyo Shirika lake litaendelea kushirikiana na Wizara kwenye kampeni yake ya kutoa chanjo ya wanyama nchini kote inayotarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Naye Mwakilishi wa kanda ya Afrika Mashariki kutoka Shirika la kimataifa linaloshughulikia afya ya Wanyama (WOAH) Dkt. Samuel Wakhusama amesema kuwa Shirika lake limeandaa Warsha hiyo kwa kushirikiana na mashirika mengine ili kujadili namna ya kutokomeza magonjwa ya Sotoka na Mbuzi na Kondoo na ule wa kichaa cha Mbwa ifikapo mwaka 2030.
Warsha hiyo ya kujadili Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la Afya ya wanyama imeandaliwa na Shirika la kimataifa linaloshughulikia afya ya Wanyama (WOAH) na inatarajiwa kuhitimishwa Julai 18, 2024 Jijini Arusha.