
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amesema fursa za uwekezaji zilizopo katika Wilaya ya Chato ni nyingi na kuwahimiza wananchi na wawekezaji mbalimbali kuzitumia, ili ziweze kuwaletea ufanisi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Waziri Ulega amesema katika sekta ya uvuvi pekee Mhe.Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ametoa jumla ya shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya kujenga mwalo na soko kubwa la kisasa la samaki wilayani Chato, ambalo litatoa fursa za kibiashara na uongezaji thamani wa mazao ya samaki na dagaa.
Waziri Ulega amesema katika upande wa sekta ya mifugo, Wizara imejenga mnada wa mifugo wa kisasa wa Buzirayombo ambao unatoa fursa kwa wafugaji kufanya biashara zao za mifugo kisasa huku akifafanua kuwa kufuatia uwepo wa idadi nzuri ya mifugo kunatoa fursa nyingine ya kujenga kiwanda cha kuchakata nyama.







Waziri Ulega amebainisha hayo wakati akifungua Tamasha la Utalii 'Chato Utalii Festival 2023' linalofanyika wilayani Chato, mkoani Geita kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo mkoani humo.
Amesema Tamasha hilo linaambatana na maonesho mbalimbali ya fursa zilizopo mkoani humo, likiwa limebeba dhana mbalimbali za uwekezaji hasa kwa upande wa kilimo, mifugo na uvuvi, utalii, utamaduni na michezo.
Fursa nyingine Waziri Ulega alizobainisha ni pamoja ujenzi wa hoteli kubwa za hadhi ya nyota tatu hadi tano kwa kuwa viwanja vinapatikana katika wilaya ya Chato, Kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa sehemu kubwa ya wilaya ya Chato, imezungukwa na maji ya Ziwa Victoria na ujenzi wa viwanda vya Nguo kutokana na kuwepo kwa kinu cha kuchambulia Pamba.
