
Watu watano wakiwemo waendesha bodaboda na wakina mama wachuuzi wa bidhaa za matunda na mbogamboga kando ya barabara ya Boma, jirani na Kituo Kikuu cha zamani cha daladala wamejeruhiwa na watatu kati yao wana hali mbaya baada ya gari aina ya Canter kuacha njia na kuwagonga.
Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro Mkaguzi Emmanuel Ochieng amekiri kupokea taarifa za uokozi majira ya saa moja usiku na kufika eneo la tukio ambapo majeruhi wamepelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa Morogoro kwa matibabu.
Jitihada zaidi bado zinaendelea katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kupata kibali cha kuzungumza na daktari au muuguzi wa zamu pamoja na majeruhi kuzungumza nao kuhusiana na ajali hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando akiwa eneo ilipotokea ajali amesema tayari walishawataka wafanyabiashara wanaofanya biashara kando ya barabara kuu kuondoka kwa hiyari maeneo hayo kuanzia Septemba nane mwaka huu na kurudi sokoni kufanya biashara zao.
