Back to top

'GESTI ZA MIFUGO' MBIONI KUANZISHWA

24 August 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Wizara yake imejipanga kuanzisha 'gesti' za mifugo (livestock guest house) katika Ranchi za Taifa (NARCO), ili kuwapa fursa vijana na wafugaji wengine kuiweka mifugo yao humo kwa muda maalum ili kuiongezea thamani na kisha kuiuza kwa bei nzuri ndani na nje ya nchi.

Waziri Ulega aliyasema hayo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya hali ya sekta ya mifugo nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kilichofanyika Jijini Dodoma.

Amesema Serikali ipo katika mpango wa kuweka miundombinu mizuri ikiwemo majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo itakayowawezesha wafugaji kufanya shughuli zao za unenepeshaji wa mifugo na kuivuna ili kukuza kipato chao.

Ameongeza kuwa wataweka utaratibu mzuri wa kuwapata vijana na wafugaji wengine ambao watakuwa tayari kupeleka mifugo yao katika gesti hizo lengo likiwa kuwafanya wafugaji waone tija ya ufugaji wa kisasa na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa ukiwaingiza matatizoni kila uchao.

Amefafanua kuwa kwa kuanza wataweka miundombinu hiyo katika Ranchi ya Mkata iliyopo Mkoani Morogoro ili kuwapa nafasi wafugaji waliopo katika Bonde la Mto Kilombero waweze kufanya ufugaji wao humo ili waondokane na ufugaji holela.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. David Kihenzile alisema kuwa mpango huo ni mzuri hivyo Wizara ifanye haraka uanze kuutekeleza kwa gharama nafuu huku akiongeza kuwa ni muhimu wizara kuona uwezekano mpango huo kuenea nchi nzima ili vijana na wafugaji wengine waweze kunufaika nao.