Back to top

Halmashauri Mwanza zitenge maeneo ya uwekezaji viwanda.

07 April 2022
Share

Serikali imeziagiza halmashauri zote za mkoa wa Mwanza kuhakikisha zinatenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na hoteli za kitalii na za kati ili kufungua milango ya kiuchumi kutokana na mkoa huo kuwa lango kuu la kuingia na kutoka katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

Agizo hilo la serikali limetolewa na mkuu wa amkoa wa Mwanza , Mhandisi Robert Gabriel kwenye mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati mkoani Mwanza katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo imeelezwa ujenzi wa viwanda vya kutosha pamoja na hoteli itasaidia kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao baaadhi ya wakazi waa jiji la Mwanza wameiomba serikali kuboresha sekta za uvuvi na wajasiliamali wadogo kwa kuwajengea maeneo bora na salama ya kuanikia dagaa ili kuondokana na changamoto ya kuuza dagaa wenye mchanga na kusababisha kukataliwa sokoni.

Aidha Mhandisi Gabriel amesema serikali haitawavumilia baadhi ya watu wachache wanaotumia vibaya fedha za miradi ya kimkakati na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi huku mkurugenzi wa jiji la Mwanza Sekiete Yahya akisema kuwa tayari jiji limeanza upimaji wa maeneo kwa ajili ya uwekezaji waa viwanda pamoja na hoteli za kitalii na za kati.