Back to top

Hatua ya awali ya rufaa ya kupinga ushindi wa wadau wa habari yaanza.

13 February 2020
Share

Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  Kitengo cha Rufaa imeanza hatua za awali za kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na serikali kupinga  ushindi wa wadau wa sekta ya habari waliokuwa  wanalalamikia  kukandamizwa  kwa uhuru wa habari kwenye kesi namba tano ya mwaka 2019.

Katika kesi hiyo namba tano ya mwaka 2019 wawakilishi wa walalamikaji ambao ni Baraza la Habari Tanzania MCT, kituo cha sheria na haki za binadamu ,na mtandao wa  watetezi wa haki za binadamu Tanzania walishinda baada ya mahakama ya Jumuiya ya Afika mashariki kutoa mamuzi  yaliyoonyesha kuwa hoja za upande  wa  walalamikaji  zilikuwa na msingi jambo lililopelekea upande wa  walalamikiwa ambao ni serikali  kuonyesha  nia ya kukata rufaa.

Hata hivyo baada ya serikali kukata rufaa  hiyo upande wapili wa wadau wa habari waliwasilisha pingamizi  ya rufaa  hiyo  kwa  madai  kuwa baadhi ya taratibu zimekiukwa ikiwemo ya kuwasilishwa nje ya muda unaotakiwa kisheria huku upande  wa serikali  nao  wakidai  kuwa  wana  sababu  za msingi  na zinazokubalika za kuchelewa kwa kuwasilisha rufaa hiyo.

Kufuatia mapingamizi hayo  jopo la majaji watano wa mahakama hiyo  Kitengo cha Rufaa  wakiongozwa na Rais wa mahakama hiyo  DK.  Emanuel Ugirashibuje  wamekutana na wanasheria wa pande zote mbili na kuweka makubaliano ya kuanza kusikiliza mapingamizi hayo .

Katika kikao hicho  baadhi ya wanasheria wa wadau wa habari akiwemo Mpale Kaba Mpoki na Jebra Kambole wamesema wamekubaliana kila upande kuwasililsha hoja zake kwa maandishi ambapo upande  wa wadau wa habari watawasilisha  hoja zake  tarehe 04/03/2020 na  upande wa serikali  watatakiwa kujibu tarehe 24/03/2020.