Back to top

IFAD KUENDELEA KUSAIDIA MIRADI YA KILIMO NA UVUVI

29 May 2024
Share

Kufuatia changamoto ya huduma ya fedha inayowakabili wakulima wengi nchini hasa wale wadogo, Serikali pamoja na  Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) wamekubaliana kuingiza miradi itakayosaidia upatikanaji wa fedha kwa wakulima wadogo  katika program mpya itakayoanza Januari, 2025 ili waweze kuendeleza miradi yao ya kilimo.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry baada ya kikao kati ya Tanzania na Mfuko huo, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024  ya Bodi ya Magavana wa Benki ya AfDB inayofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya.

Dkt. Mwamba alisema Mfuko huo umekuwa ukiendelea kusaidia miradi mbalimbali ya kilimo na uvuvi nchini kwa pande zote mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mshiriki anayeshughulikia miradi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Donal Brown, alisema IFAD kupitia miradi yake mbalimbali inalenga kuinufaisha jamii hasa kwa wale wanaoishi vijijini ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu inayohusiana moja kwa moja na kilimo cha biashara.

Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umekuwa ukifanya kazi na Serikali ya Tanzania ili kuendeleza sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini ili kufikia uzalishaji wa juu, endelevu na kibiashara. Ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya wakulima wadogo na kuboresha upatikanaji wa masoko.