
Ilani mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha 2025–2030, imeelezwa kuwa dira ya maendeleo Jumuishi kwa Watanzania, ikilenga kuchochea uchumi wa kisasa, kuongeza ajira, kuboresha huduma za jamii na kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa kupitia Diplomasia ya Uchumi.
Afisa wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Abdallah Kirungu, ambaye pia aliwahi kuwa Afisa Mwandamizi Mkuu wa Ubalozi Mdogo wa Tanzania Dubai, amesema Ilani hiyo imejikita katika maeneo yote muhimu ya maisha ya Mtanzania, yakiwemo elimu, afya, maji, kilimo, miundombinu, ulinzi na usalama, michezo, na utamaduni.
Kwa mujibu wa Kirungu, moja ya maeneo yaliyopewa uzito mkubwa ni Diplomasia ya Uchumi, ambapo amesema kuwa ilani hiyo inalenga kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kutetea maslahi ya Taifa na kuongeza uwekezaji.
"Sera ya Mambo ya Nje ni mwendelezo wa sera za ndani ya nchi na ni nyenzo muhimu inayotumika kujenga na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kijamii na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa"Amesema Kirungu.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi unatekelezwa kikamilifu kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo ni nguzo kuu katika kufanikisha malengo ya kimkakati yaliyomo kwenye Ilani ya CCM 2025–2030.
Kirungu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa mujibu wa utaratibu wa kimataifa ni Mwanadiplomasia Namba Moja wa Taifa, kwa kuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia ushiriki wake kwenye majukwaa ya kikanda na kimataifa.
"Mheshimiwa Rais amekuwa kinara katika kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye masuala ya uchumi, nishati, usalama na diplomasia. Ziara zake nje ya nchi zimeleta mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji"Amesema na kuongeza.
"Ni muhimu Watanzania wakatambua kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa na ya kipekee katika kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo kupitia ushiriki wake katika majukwaa ya kimataifa".