Back to top

IMF imesema ipo tayari kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania.

03 May 2021
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bi. Kristalina Georgieva kuhusu ushirikiano kati Tanzania na IMF katika masuala ya kiuchumi.

Mhe. Rais Samia aliyekuwa ofisini kwake Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma amemshukuru Bi. Kristalina aliyekuwa nchini Marekani kwa ushirikiano na ufadhili mkubwa ambao IMF umeutoa nchini Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa lengo la kuendelea kujenga uchumi imara wa Tanzania.

Kwa upande wake Bi. Kristalina amempa pole Mhe. Rais Samia kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia kuwa IMF ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi.

Bi. Kristalina amesema IMF ipo tayari kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyopata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na janga la Corona zikiwemo sekta za utalii, afya, uzalishaji na huduma za kijamii na amebainisha kuwa shirika hilo litafanyia kazi mara moja maombi ya mkopo nafuu kutoka Tanzania.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili, IMF imepanga kutumia Dola za Marekani Bilioni 650 kwa ajili ya kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi zinazoendelea zilizopatwa na madhara ya Corona.

Kufuatia ahadi hiyo, Mhe. Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambao wamehudhuria katika mazungumzo hayo kukamilisha haraka mchakato wa maandiko ya kuomba mkopo nafuu kutoka IMF ili fedha hizo zisaidie kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.