Back to top

JAFO apigilia msumari uchaguzi serikali za Mitaa.

09 November 2019
Share

Waziri wa TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo amesema uchaguzi wa serikali za Mitaa utafanyika kama ulivyopangwa, huku akisema vyama vilivyojitoa havitazuia zoezi hilo kuendelea.

Mhe.Jafo amesema serikali imeshapokea zaidi ya rufaa 13, 500 nchi nzima, ambapo mpaka sasa wagombea waliojitokeza na kuchukua fomu ni 550, 036 na waliorejesha fomu hizo kwa wakati ni 539, 953 sawa na asilimia 97.29.

Mhe.Jafo ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo leo ndio siku ya mwisho ya kumaliza rufaa kwa wagombea waliopeleka malalamiko yao kwenye kamati hizo ambazo zinasimamiwa na Makatibu Tawala wa Wilaya.

Wakati zoezi hilo likielekea ukingoni, Tayari vyama vitatu vya siasa nchini Tanzania, CHADEMA, ACT Wazalendo na CHAUMA vimeshajiengua kwenye mchakato huo wa uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019, kwa kile wanachodai wanachezewa rafu.