
Wazazi wa binti wa miaka 18 raia wa Pakistan, wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na mjomba wake amehumukiwa miaka 14 jela, baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya binti huyo nchini Italia baada ya kukataa matakwa ya familia yake ya kuolewa na binamu katika nchi yao.
Mwili wa Saman Abbas ulifukuliwa Novemba 2022 katika shamba lililotelekezwa, karibu na shamba ambalo baba yake alikuwa anafanya kazi Kaskazini mwa Italia, mwaka mmoja na nusu baada ya kuonekana hai kwa mara ya mwisho kwenye video akiwa na wazazi wake.
Waendesha mashtaka wa Italia walidai kwamba aliuawa na familia yake tarehe 1 Mei 2021. Siku chache baadaye, wazazi wake walisafiri kwa ndege kutoka Milan hadi Pakistan.
Siku ya Jumanne, wazazi hao, Shabbar Abbas na Nazia Shaheen, walihukumiwa kifungo cha maisha jela, huku mjomba wake, Danish Hasnain, akihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela.
