
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 4 Machi 2022 akiwa Nairobi nchini Kenya ametembelea eneo la Upper Hill ambapo kuna kiwanja cha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachotarajiwa kujengwa jengo la Ghorofa 23 la Ubalozi na kitega uchumi cha Ubalozi.

Akizungumza mara baada ya kukagua eneo la ujenzi wa jengo hilo unaotarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka 2022 na kukamilika baada ya miaka mitatu Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha ujenzi huo unaanza mara moja kama ilivyopangwa.
Amesema tayari serikali iimetoa fedha za ujenzi hivyo mkandarasi anapaswa kuendana na kasi ya ujenzi lakini kwa kuzingatia ubora.
Amesema uwepo wa jengo hilo utawezesha Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya kujiendesha pamoja na kutumika kuendesha balozi zingine katika maeneo mbalimbali kwa kutumia kitega uchumi hicho.
