Jeshi la polisi lawaonya madereva waliopanga kufanya mgomo.

Jeshi la polisi nchini limewatahadharisha madereva wote wa mabasi ya abiria waliopanga kufanya mgomo kuanzia January tisa mwaka huu kwa madai ya kuwa wanaonewa na askari wa usalama barabarani wasitishe mgomo huo na kuendelea kutoa huduma kwa abiria na kwamba yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi

Akizungumza jijini Dodoma msemaji wa jeshi la polisi nchini SACP David Misime amesema kumekuwepo na taarifa za madereva wa mabasi ya abiria ambao wamepanga kugoma kutokana na malalamiko mbalimbali ambapo kamanda Misime amewataka madereva hao kusitisha mgomo huo kwani malalamiko yao yameshapekwa sehemu husika kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi na kuyatatua.

Aidha katika hatua nyingine kamanda Misime ameelezea hali ya usalama nchini ambapo amesema katika kipindi cha miaka minne matukio ya ajali za barabarani yameendelea kupungua ambapo amesema jeshi la polisi linaendelea kutoa elimu kwa madereva katika kuhakikisha wanapunguza ajali za barabarani.