
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wananchi wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, kujitokeza kwa wingi kuomba maeneo yao ya ardhi kutambuliwa.
Mhe.Pinda ametoa kauli hiyo katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wananchi waliotambuliwa kupitia mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Manyara.
Jumla ya wamiliki wa ardhi 68 katika wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara walikabidhiwa hati milki za ardhi zilizopatikana kupitia mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK).



Ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Mbulu kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na migogoro mikubwa ya ardhi na kubainisha kuwa iwapo maeneo yote ya wilaya hiyo yatapimwa migogoro ya ardhi itakwisha yenyewe.
Vile vile, Naibu Waziri wa Ardhi amewahimiza wananchi wa Mbulu kuchangamkia hati zinazotolewa kupitia mradi wa KKK huku akiitaka ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara kuhakikisha inahamasisha wananchi kujua ubora na matumizi ya hati.
Sambamba na suala hilo, Mhe, Pinda ameelezea kuwa, uwepo wa Klinik za ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini ni sehemu ya juhudi za wizara yake kushughulikia migogoro ya ardhi.
Amemtaka Msajili wa Hati na Nyaraka wa mkoa wa Manyara kuhakikisha anaharakisha utoaji wa hati kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu ili kuwaondolea usumbufu.
