
Waziri Mkuu wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni ili kujumuisha baadhi ya watumishi wa umma waliopo katika sekta nyeti kujaza fomu ya Tamko la Rasilimali na Madeni.
Mheshimiwa Nchemba ametoa agizo hilo jijini Dodoma alipofanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya taasisi hiyo ili kujionea shughuli zinazotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili na kutoa uelekeo wa maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi.

Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa zipo baadhi ya sekta ama nyadhifa mbalimbali za watumishi ambazo ni kitovu cha ukiukwaji wa maadili unaosababisha upotevu na ubadhilifu wa fedha za Umma, lakini watumishi wa sekta hizo hawawajibiki na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995 inayowataka Viongozi wa Umma kujaza Fomu ya Tamko la Rasilimali na Madeni.
“Tunaweza kuwa tunatekeleza kikamilifu suala la usimamizi wa matamko kwa viongozi wa umma , lakini uhalisia wake masuala ya ukosefu wa maadili yakaendelea nchini,” amesema na kuongeza kuwa, “maeneo ambayo fedha ya umma zinapotea ni manunuzi ya umma, eneo la makusanyo hasa watumishi wanaohusika na makadilio ya kodi, maafisa wanaohusika na mikataba, utoaji wa leseni za madini, sekta ya ardhi, wajumbe wa zabuni, ukaguzi na udhibiti hivi ndivyo vyanzo vikubwa vya upotevu wa fedha za Serikali,” ameeleza.
Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ina majukumu kubwa, nyeti na mazito katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinalindwa.
“Tunataka kuona Taasisi hii inakuwa kimbilio kwa kila mtu anayeona kuna ukiukwaji wa maadili, kila mwananchi aamini kuwa akifika katika Taasisi hii atapata ufumbuzi wa changamoto yake hivyo, niwaase kusimamia maadili kwa kiwango cha juu. Mtu ambaye hataki kuwa na nidhamu binafsi, sisi Serikali tumlazimishe.
Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Mkuu aliongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) pamoja na Katibu Mkuu Ikulu Bw. Majula Mahendeka.
