Back to top

Kalemani asema hali ya upatikanaji umeme nchini kwa sasa ni nzuri.

27 February 2021
Share

Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani amesema hali ya upatikanaji umeme nchini kwa sasa ni nzuri ambapo wana ziada kutosha.

"Tuna megawati 1,604 wakati matumizi ya Watanzania,ni megawati 1,180 hivyo zaidi ya megawati 400 ni ziada"amesema.

Kauli hiyo ya Dk.Kalemani ameitoa wakati wa semina iliyoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyohusisha wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo vya habari mbalimbali inayofanyika mkoani Morogoro.

Amesema hali halisi kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ni nzuri katika mabwawa yote saba ya kuzalisha umeme, kwa mfano bwawa la Mtera limejaa kufikia kikomo chake cha ujazo 698.76, huku akieleza kwamba anatarajia kulifungulia bwawa hilo hivi karibuni, kupunguza maji kwa lengo la kuilinda miundombinu.

"Bwawa la Kidatu limejaa kufikia mita za ujazo 448.81 wakati uwezo wake ni mita za ujazo 450"-Dkt.Kalemani.

Akizungumzia Mradi wa Kuzalisha Umeme Julius Nyerere (JNHPP) Waziri Kalemani amesema unaendelea vizuri, kazi zote tano muhimu za ujenzi zinaendelea vyema na mkandarasi ameshalipwa zaidi ya shilingi trilioni 1.9 sawa na zaidi ya asilimia 100 aliyotakiwa kulipwa.

Amebainisha faida za mradi mbali na umeme wa uhakika, utasaidia kuokoa mazingira ikiwemo ukataji miti ambapo akitolea mfano Jijini Dar es Salaam magunia ya mkaa kati ya 400,000 mpaka 500,000 yanatumika.

JNHPP mpaka sasa imeshazalisha ajira zaidi ya 7,000 za moja kwa moja na zisizizo za moja kwa moja.

Ujenzi wa Mradi wa JNHPP unaenda sambamba na kufunga minara ambapo hadi sasa wameshafunga minara 456 ya umeme na kipande cha Dar es Salaam hadi Kingolwira, kimekamilika kinachosubiriwa ni majaribio.

"Megawati 70 za umeme zimeshatengwa kwa ajili ya SGR hivyo hakuna cha kukwamisha mradi huo kwenye nishati hata kama ungeanza leo"- amesema Waziri Kalemani.