
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeisisitiza Serikali kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi na kuendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto za Wakandarasi hao, ili kutoa fursa ya ushindani na Wakandarasi wa nje katika upatikanaji wa zabuni.
Hayo yameelezwa Mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe.Selemani Kakoso wakati Kamati hiyo ilipokagua maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa vivuko vinavyojengwa na Mkandarasi Mzawa Songoro Marine.
"Hakikisheni mnawajali wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi kwa kuwapatia malipo kwa wakati, mkimuwezesha Mkandarasi huyu ataenda kuwekeza katika Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika na kuleta ajira kwa wananchi wa maeneo husika" Kakoso.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiahidi Kamati kufuatilia malipo ya Mkandarasi Mzawa Songoro Marine, ili akamilishe ujenzi wa vivuko vipya vitano pamoja na ukarabati wa vivuko viwili.
"Nitahakikisha nafuatilia kwa ukaribu malipo haya Wizara ya Fedha (HAZINA), na naamini kuwa fedha zitapatikana na Mkandarasi ataendelea na utekelezaji wake kama ilivyopangwa"Amesisitiza Bashungwa.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bw.Lazaro Kilahala, ameeleza kuwa Wakala huo unaendelea kusimamia ujenzi na ukarabati wa vivuko hapa nchini ili kuongeza utoaji wa huduma za usafiri kwa wananchi.
