Back to top

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU

12 October 2023
Share

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa mafanikio makubwa katika kutekeleza afua za VVU na UKIMWI nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo, wakati kamati ilipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Mpango wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC), unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360), kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) katika katika Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza mara baada ya kukagua vikundi vya vijana  vikiwemo  Sitetereki kilichopo Kata ya Old Shinyanga, Jahazi, Kata ya Ibadakuli na Tunaweza katika Kata ya Kolandoto Mhe. Nyongo amesema lengo la ziara ni kujionea maendeleo ya mradi huo na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewaomba vijana wa kike kuendelea kujiamini na kufanya kazi vizuri kwani Serrikali ya Awamu ya Sita inawajali vijana na kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa.