
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifungo, imetembelea miradi ya ujenzi miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo mradi wa bwawa la Msagali, Membe pamoja na Chinangali, iliyopo wilaya ya Mpwapwa na Chamwino mkoani Dodoma na kuridhishwa na hatua za utekelezaji wa miradi hiyo na kushauri kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ijumuishe uibuaji wa fursa nyingine za kiuchumi, kupitia utalii wa kilimo.
Kamati hiyo iliaambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde na Mkurungezi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw.Raymond Mndolwa, ambapo Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.Mariam Ditopile (Mb ), amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ikiwemo bilioni 27 kwa ajli ya ujenzi wa bwawa la Msagali.
Mhe.Ditopile, ameipongeza Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa usimamizi thabiti na utekelezaji, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo kwa asilimia kubwa miradi hiyo imefika katika hatua nzuri za utekelezaji.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.David Silinde amebainisha kuwa mageuzi makubwa yanayofanywa na serikali katika sekta ya kilimo kufikia lengo la ajira milioni nane kupitia kilimo cha kisasa na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja hasa kupitia mpango wa taifa wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT).



Akizungumza na kamati hiyo katika bwawa la Msagali, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa amesema bwawa hilo litatumika kumwagilia eneo lenye ukubwa wa ekari 1,250, ambapo bwawa hilo litakuwa na ujazo wa lita bilioni 92, ambayo maji yake yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji, mifugo pamoja na matumizi ya binadamu.
Mradi wa bwawa la Msagali, unatekelezwa katika kata ya Ng’ambi na Chunyu tarafa ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma ikiwa ni miongoni mwa miradi ya kimakakati, inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita, chini mheshimiwa rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, kamati hiyo imehitimisha ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa shughuli za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji , katika mkoa wa Dodoma ambapo, miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Msagali, Chinangali, Ndogowe pamoja na bwawa la Membe.
