Back to top

KAMATI YA BUNGE YATOA KONGOLE UTEKELEZAJI MRADI WA KKK MERU

16 March 2023
Share

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imepongeza Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) unaotekelezwa na Halmashauri ya Meru katika shamba la Valeska lililokuwa linamilikiwa na Chama cha Ushirika cha mkoa wa Arusha (Arusha Cooperative Union Ltd-ACU) katika mkoa wa Arusha.

Chama cha Ushirika cha mkoa wa Arusha (ACU) kilishindwa kuendeleza shamba hilo na kupelekea kufutwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Mei 2018 kwa mujibu wa kifungu namba 45 cha Sheria ya Ardhi na ufutwaji huo kusajiliwa Sept 27, 2018.

Maelekezo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusiana na eneo la shamba hilo ni kwamba vijiji vinavyozunguka shamba la Valeska ambavyo ni Kwaugoro, Maroroni na Valeska ni kutengewa ekari 500 kwa kila kijiji kama mpango wa mgawanyo wa shamba ulivyopendekeza.

Akizungumza wakati wa ukaguzi utekelezaji mradi wa KKK katika eneo la Valeska Machi 16, 2023 mkoani Arusha, mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii  Timotheo Mzava aliipongeza halmashauri ya Meru kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kueleza kuwa halmashauri hiyo ni ya mfano kati ya halmashauri mbalimbali nchini zilizokopeshwa fedha na wizara ya Ardhi.

"Hapa niipongeze sana serikali na hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya ikiwemo kutoa fedha za kupanga kupima na kumilikisha ardhi  ambapo Meru imekuwa mfano kwa kazi nzuri waliyoifanya". Alisema Mzava

Mbunge Festo Sanga ametoa pongezi kwa halmashauri ya Meru kwa utekelezaji mzuri wa  project ya KKK na kueleza kuwa  kilichofanyika ni moja ya kitu kikubwa kilichofanywa na halmashauri nchini na kueleza kuwa halmashauri nyingine nchini  zina cha kujifunza kupitia mradi huo wa KKK  na Meru ni kielelezo na mfano.