
Kamati za uratibu wa Maafa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji zimetakiwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu katika kuzuia, kupunguza vihatarishi na kuwa tayari kukabiliana na maafa ili kuleta maendeleo endelevu kwa Wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Meja Jenerali Michael Mumanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Dkt.John Jingu wakati wa hafla ya kushuhudia utiaji saini na kukabidhi Mkakati wa kupunguza vihatarishi vya maafa pamoja na Mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa iliyofanyika katika Halmashauri Wilayani Rufiji moani Pwani.
Amesema jamii ya Rufiji imekuwa ikihitaji muitikio mkubwa wa Serikali na wadau katika usimamizi kutokana uwepo wa majanga ya maafuriko, migogoro kati ya wakulima na wafugaji, ukame, magonjwa ya mlipuko, wanyama pori pamoja na wadudu waharibifu.

Pia alitoa shukurani kwa Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) kwa ufadhili wa kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa mpango wa kujiandaa kukabiliana na maafa katika bajeti kwa Halmashauri mbalimbali Nchini.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Bwa.John Kayombo alibainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imechukua hatua za kuandaa mpango wa kujiandaa na kukabili maafa baada ya kufanikiwa kufanya tathimini ya vihatarishi.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Meja Edward Gowele aliahidi kutekeleza mpango huo kwa kushirikiana na kamati, kusimamia na kuufanyia kazi mpango huo.
