
Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel ameagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizopo pembezoni mwa nchi kuweka utaratibu endelevu wa kuwa na kambi za kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Dkt.Mollel ametoa agizo hilo leo akiwa wakati wa uzinduzi wa Kambi ya Huduma za Kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni Kigoma na kujionea hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Huu utaratibu wa madaktari wetu bingwa kutoka hospitali za kibingwa kuwafuata wananchi waliopo kwenye Mikoa iliyopo pembezoni na kuhudumiwa huko utakuwa ni utaratibu endelevu na kwa maeneo yote ya pembezoni katika nchi yetu" amesema Dkt. Mollel.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuboresha Sekta ya Afya nchini kwa kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za afya, ununuzi wa vifaatiba pamoja na kusomesha watalaam wa afya ndani na nje nchi huku akikiri kuwa bado tuna changamoto ya uhaba wa wataalam wa kibingwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Hata hivyo Dkt. Mollel amesema kuwa kambi hizo za madaktari bingwa kuwepo kwenye maeneo hayo ya mbali kutawasaidia wananchi kuokoa fedha ambazo wangezingetumia kwenda umbali mrefu kufuata huduma za tiba.
Aidha amepongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kusimamia vyema ujenzi wa miundombinu inayoendelea kujengwa katika Hospitali hiyo ambayo itawawezesha wataalam hao bingwa kuweza kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
