Back to top

KAMPENI YA ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI ZIWA TANGANYIKA.

18 June 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki amezindua Kampeni ya kitaifa ya Uelewa kuhusu Mkataba wa kikanda wa Usimamizi wa Uvuvi Endelevu wa Ziwa Tanganyika iliyosheheni mikakati mbalimbali ya Ulinzi wa rasilimali za Uvuvi za ziwa hilo.

Katika hotuba yake kabla ya kufanya uzinduzi huo uliofanyika kwenye Mwalo wa Kabwe mkoani Rukwa, Mhe. Ndaki amebainisha kuwa kampeni hiyo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa mkataba unaojumuisha nchi zote zinazonufaika na Uvuvi wa Ziwa Tanganyika ambazo ni Tanzania, Burundi, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo

"Sote tunafahamu kuwa samaki hawana mipaka na huwezi kuwapangia maeneo ya kwenda ndani ya ziwa hivyo tukaona ni vema tukawa na mwongozo wa pamoja baina ya nchi hizi zinazohusika na Ziwa Tanganyika ili tuwe na lugha moja kwenye utekelezaji wa kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa kwa wavuvi waliopo kwenye nchi husika". Amesema Ndaki.

Aidha Mhe.Ndaki amewaagiza watalaam wote wa Sekta ya Uvuvi waliopatiwa semina elekezi kuhusu mkataba huo kuhakikisha wanafikisha elimu kwa wavuvi ambao ndio walengwa wa mkataba huo ili wauelewe kabla ya kuanza kuutekeleza.

"Mkaitishe mikutano ya wavuvi moja kwa moja mkawaelimishe, msiishie kwa viongozi wa kata au Serikali za vijiji kwa sababu mara nyingine viongozi hao hawaendi ziwani na hata changamoto za wavuvi hawazijui" Amesisitiza Mhe.Ndaki.

Mhe. Ndaki ametoa rai kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi wa Ziwa Tanganyika kuwa tayari kujitokeza kwa wingi pindi wakihitajika kwa ajili ya kupewa elimu kuhusu mkataba huo ili waweze kutoa maoni yenye lengo la kuuboresha kabla ya kuanza kuutekeleza.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko amesema kuwa miongoni mwa changamoto ambazo zilikuwa zikiikabili sekta ya Uvuvi kwenye mikoa inayopitiwa na ziwa Tanganyika ni utoroshwaji wa rasilimali za uvuvi kwenda nje ya nchi kupitia maeneo ya mipakani na baadhi ya wavuvi kuvamiwa na kuporwa mali zao hivyo anaamini mkataba huo utaondoa changamoto hizo.

Akizungumzia kiwango cha samaki wanaovuliwa katika ziwa hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi Dkt.Rashid Tamatamah amesema kuwa Ziwa Tanganyika huchangia takribani asilimia 19 ya samaki wote wanaozalishwa nchini ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 ziwa hilo lilizalisha tani 90,743 zenye thamani ya shilingi bilioni 592.5.

Naye Mkurugenzi wa Kanda wa Uvuvi na ufugaji wa samaki kutoka mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Beatrice Marwa amebainisha kuwa uvuaji wa samaki wachanga katika ziwa hilo kwa upande wa Tanzania unasababisha upotevu wa zaidi ya dola 690,000 za Marekani kila mwaka huku nchi ya Zambia ikipoteza zaidi ya dola 1,000,000 za Marekani kutokana na kitendo hicho.

Uzinduzi wa kampeni hiyo hapa nchini umefanyika mara baada ya nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Zambia na Burundi kufanya hivyo takribani wiki mbili zilizopita lengo likiwa ni kuunganisha nguvu ya pamoja katika ulinzi wa rasilimali za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika na kuufanya uvuvi huo kuwa endelevu.