Back to top

Kampuni ya Barrick yailipa serikali dola milioni 100.

26 May 2020
Share

Kampuni ya Barrick imeilipa Tanzania dola milioni 100, sawa na takriban sh. bilioni 250, ikiwa ni sehemu ya malipo ya dola milioni 300 ambazo Kampuni hiyo ya Madini ilikubali kulipa kama fidia ya kodi.

Mfano wa Hundi ya kiasi hicho cha fedha umetolewa na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick, Bw. Hilaire Diarra kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip  Mpango, kwa niaba ya Serikali jijini Dodoma leo.

Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano na Barrick ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na Kamati yake, Dkt. Mpango alisema tukio hilo ni  mwanzo wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo yaliyofikiwa Disemba 19, 2019 na kusainiwa rasmi Januari 24, 2020.

Dkt. Mpango aliyataja makubaliano mengine yaliyofikiwa kati ya Serikali na kampuni hiyo kuwa ni kuundwa kwa Shirika la Madini la Twiga lenye umiliki wa pamoja litakalofanya kazi nchini katika kusimamia uendeshaji wa migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara pamoja na migodi mingine nchini ambapo Serikali ya Tanzania itashiriki katika utoaji wa maamuzi kuhusu uendeshaji wa migodi, mipango, manunuzi pamoja na masoko ya madini.

Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Dennis Mark Bristow ambaye alikuwa akifuatilia makabidhiano hayo kwa njia ya mtandao na kutoa hotuba yake akiwa nchini Afrika Kusini alimpongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Timu yake kwa kufanikisha majadiliano yaliyosaidia kuanzishwa kwa ushirikiano wa dhati kati ya Kampuni yake na Serikali.