
Serikali imeuelekeza uongozi wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania ambayo inajenga meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu kuzingatia makubaliano yote yaliyomo kwenye mkataba wa ujenzi wa meli hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa katika kikao kati yake na Balozi wa Korea ya Kusini nchini, Kim Sun Pyo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam.
Katika Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania Bw. Kwak ambaye alikiri mapungufu katika utekelezaji wa mradi huo na aliahidi kuwa kampuni yake itaongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kwa wakati na meli hiyo iwezo kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.
Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelekeza kuwa watalaamu wa Kampuni ya Gas Entec Tanzania warejeshewe Pasi zao za kusafiria ambazo zilizuiwa na serikali kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mwenendo wa ujenzi wa meli hiyo.