Back to top

KAPINGA: VITONGOJI 33,000 VYAFIKIWA NA HUDUMA YA UMEME.

21 June 2024
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata umeme ambapo mpaka sasa vitongoji  33,000 vimesambaziwa umeme kati ya vitongoji zaidi ya 60,000.

Mhe. Kapinga amesema hayo tarehe  21 Juni 2024,  Bungeni  Jijini Dodoma wakati akijibu maswali mbalimbali ya  Wabunge katika kipindi cha Maswali na Majibu.

Kapinga amesema kutokana na suala la maendeleo  kuwa ni  hatua,  Serikali iliweka nguvu kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na sasa hatua inayofuata ni kupeleka umeme vitongojini ili kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi.
 
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Mhe. Edwin Swale kuhusu mpango wa Serikali kupeleka umeme wa REA kwenye Vitongoji, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Lupembe lina vitongoji 227 ambapo vitongoji 118 vimekwishapatiwa umeme na vitongoji 109 vilivyobaki Serikali pia itavipelekea umeme.

Ameongeza kuwa, vitongoji 19 kati ya hivyo vitapatiwa umeme kupitia mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu. Vile Vile, vitongoji 15 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Vitongoji 15 kila Jimbo, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni. 

Aidha, Vitongoji  75 vitapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa “Hamlet Electrification Project” ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/25 kulingana na upatikanaji wa fedha.

Akizungumzia Kijiji cha Madeke na maeneo ya uwekezaji katika mji wa Njombe kupatiwa umeme Mhe. Kapinga  amesema Serikali itafuatilia ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuwasimamia kwa umakini mkubwa wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi zao kwa wakati na kwa ufanisi.

Akijibu swali la Mhe. Yahaya Masare, Mbunge Jimbo la Manyoni Magharibi kuhusu kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 vya Halmashauri ya Itigi, Mhe. Kapinga amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo, ikiwa ni  kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema kupitia  mwaka wa fedha unaokuja wa 2024/25, Serikali imetenga fedha za kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000.

Akijibu swali la Mhe. Minza Mjika, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu aliyetaka kufahamu ni lini vitongoji ambavyo havina umeme katika  Mkoa wa Simiyu vitapata umeme, Mhe. Kapinga amesema ipo miradi inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa ujazilizi na kuongeza kuwa,  kutokana na Serikali kuona umuhimu wa umeme kwa wananchi imebuni miradi mbalimbali itakayotimiza dhamira ya Serikali ya  kila mwananchi kupata huduma ya umeme.

Akijibu swali la Mhe. Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum ambaye alitaka kufahamu kuhusu umeme kufika kwenye baadhi ya Kata ambazo zipo vijijini katika Jimbo la Bunda mjini kati ya kata 14 kata 7  zipo Vijijini,  Mhe. Kapinga amesema kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imefanya utaratibu wa kuhakikisha mitaa ya Bunda mjini ambayo haina umeme inapata umeme na itaendelea kupeleka umeme hadi kwenye vitongoji. 

Aidha, aikibu swali la nyongeza kutoka kwa Mhe. Daimu Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kuhusu lini Mkandarasi anayetekeleza miradi ya ujazilizi ataanza kazi, Mhe. Kapinga amesema kutokana na kuelekea kukamilika kwa miradi ya umeme vijijini, hivi karibuni inaanza miradi ya ujazilizi katika Vitongoji vya jimbo la Tunduru Kusini. 

Aidha, kuhusiana na Vijiji vingine kurukwa kupatiwa umeme Mhe. Kapinga Wabunge kuwa maendeleo ni hatua hivyo maeneo yote yatafikiwa na umeme kwa awamu.