Back to top

SEKTA YA MAWASILIANO NI NGUZO KUU YA UCHUMI AFRIKA

05 May 2026
Share

Mkuu wa Udhibiti wa Airtel Africa na Mwenyekiti wa Kundi la Sera Afrika la GSMA, Bw. Daddy Mukadi, amezitaka serikali za Afrika kuitambua sekta ya mawasiliano ya simu kama nguzo kuu ya uchumi, huku akipendekeza mageuzi mawili muhimu ya kodi yatakayochochea kwa kasi ujumuishaji wa kidijitali barani.

Amesisitiza kuwa sekta ya mawasiliano haipaswi tena kuonekana kama sekta saidizi, bali mhimili mkuu wa maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Amebainisha haya katika mkutano wa kwanza wa États Généraux du Secteur des Postes et Télécommunications uliofanyika Kinshasa, Mukadi na kueleza kwamba ni wakati wa wadau wa serikali na sekta binafsi kubadili mtazamo kuhusu nafasi ya sekta ya mawasiliano. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix Tshisekedi.

Kauli hiyo inakuja wakati uchumi wa kidijitali barani Afrika ukiendelea kukua kwa kasi. Kwa mujibu wa ripoti ya Mobile Economy Africa 2025 ya GSMA, sekta ya simu ilichangia dola za Marekani bilioni 220 katika uchumi wa Afrika mwaka 2024, sawa na asilimia 7.7 ya Pato la Taifa (GDP). Inakadiriwa kufikia dola bilioni 270 ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto bado ipo ingawa mitandao ya simu inafikia takribani asilimia 95 ya watu barani Afrika, karibu asilimia 75 bado hawatumii intaneti. Sababu kubwa ni gharama za juu za vifaa vya kidijitali na huduma husika.

Mukadi amesisitiza umuhimu wa maboresho ya sera za umma pamoja na mifumo ya kisheria na udhibiti ili kupunguza gharama, kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali, na hatimaye kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali barani Afrika.