Back to top

Kesi ya Mbowe na wenzake yaendelea kusuasua Kisutu.

21 August 2018
Share

Wakili Peter Kibatala anayewatetea viongozi waandamizi wa CHADEMA ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuiahirisha kesi ya jinai namba 112/2018 kwa kipindi kisichozidi siku 30 kwa kuwa washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Kibatala aliyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati wa usikilizwaji wa maombi yao ambapo wanaomba kesi hiyo iahirishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa Mahakama ya rufaa.

Wakili Kibatala, alidai kuwa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ambacho ndio wametumia kuleta maombi hayo kinaipa Mahakama hiyo mamlaka ya kufanya hayo.

Katika maombi yao wanaomba Mahakama ya Kisutu iridhie kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya jinai namba 112/2018 ili kutoa nafasi kwa Mahakama ya rufaa kusikiliza na kutoa uamuzi katika maombi ya kusimama kwa kesi ya msingi iliyopo mahakama ya Kisutu na rufaa namba 215/2018.

Akijibu hoja hizo za wakili Kibatala, wakili wa serikali mkuu, Faraja Nchimbi alidai kuwa maombi hayo ya utetezi yanakosa baraka za kisheria mbele ya Mahakama hiyo.

Wakili Nchimbi aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kwa sababu yanakosa msingi wa kisheria.

Baada ya kuyasikiliza upande zote mbili hakimu Mashauri aliiahirisha usikilizwaji wa maombi hayo hadi Agosti 23, mwaka huu ambapo atatoa uamuzi kesi hiyo iahirishwe ama la.