Back to top

Kichocho na homa ya matumbo chawatesa wakazi wilaya ya Mtwara.

09 September 2019
Share

Wananchi wa kijiji cha Chekereni kata ya Kitere wilaya ya Mtwara wanakabiliwa na magonjwa ya kichocho na homa za matumbo kutokana na kutumia maji yasiyo safi na salama.

Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Kitere Amekiri kupokea wagonjwa wawili mpaka watatu kwa siku wanaougua magonjwa hayo.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho, wananchi hao wamesema licha ya kijiji chao kugundulika kuwa na maji ya kutosha ardhini, hakuna visima na hivyo kulazimika kutumia maji yasiyofaa.

Wamesema maji hayo yamekuwa yakiwasababisha waugue magonjwa hayo hivyo wameiomba serikali kuwapelekea maji safi na salama ili waweze kuondokana na adha hiyo.

Kwa upande wake Mganga  Mfawidhi wa kituo cha afya Kitere Dakta Ashar Abel amekiri kuwapo kwa maji yasiyofaa yanayotumiwa na wananchi.

Hata hivyo amesema wataalam wa afya wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi  kwa kuwataka wayachemshe maji hayo kabla ya kuyatumia, hasa kwa kunywa, elimu ambayo ni endelevu.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Bwana Omar Kipanga amesema kata ya Kitere ina mradi wa maji unaoendelea kwa sasa, hivyo chombo kipya kilichoundwa na serikali kusimamia sekta ya maji kwa sasa kinasimamia mradi huo.