Back to top

Kiongozi mzuri ni yule anayetengeneza mfumo wa idara yake-DC Muro.

23 June 2022
Share

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Jerry Muro, amewagiza viongozi wa vitongoji,vijiji na kata kujenga utamaduni wa kusikiliza kero za wananchi, kuitisha mikutano na kuwasomea mapato na matumizi kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.

Ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa madiwani, wenyeviti wa vijiji, watendaji wa  vijiji na wenyeviti wa vitongo vya kata ya Puma ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake kusikiliza kero na namna ambavyo viongozi wa maeneo husika wamewajibika kuzipatia ufumbuzi.

Muro alisema ni aibu kwa Mwenyekiti wa kijiji au kitongoji tangu achaguliwe hajawahi itisha mkutano wa hadhara kuwasomea mapato na matumizi ya kijiji wananchi wake kwani hiyo ndio inawapa wakati mgumu wakati wa uchaguzi.

"Baadhi ya viongozi wanatoa visingizo kuwa wakiitisha mikutano wananchi hawaji, kama ukiona mwenyekiti unaitisha mkutano hawaji basi ujue wewe una tatizo na sasa unatakiwa kurudi ndani ukiulize wewe na mtendaji wako mtafakari kuna nini maana haiwezekani waliokuchagua wakashindwa kukusikiliza," DC Jerry Muro.

Mkuu huyo wa wilaya alisema viongozi lazima watambue kuwa ukiwahudumia wananchi kwa kutatua kero zao ni lazima wakati wa uchaguzi watakupa kura lakini kama husikilizi shida zao ikifika kwenye uchaguzi wanakupiga chini.

"Tunahitaji kuona viongozi wanakwenda kusikiliza kero za wananchi, wanakagua miradi ya maendeleo, miradi hii ni ya kwenu sio ya DC," alisema.

Muro alisema staili ya utendaji wake wa kazi ni kuwajengea mfumo wa utendaji kwani sio vizuri kila kero hadi afike Mkuu wa Wilaya kuutatua hali ikifika hapo ujue mfumo haufanyi kazi.

"Kiongozi mzuri ni yule anayetengeneza mfumo wa idara yake ili mfumo ufanye kazi na sio yeye, mfumo ukifanya kazi hata yeye kichwa kitapungua lakini ikiwa kila kitu DC mwisho wa siku ikifika wakati wa uchaguzi utataka aje akuombee kura sababu kazi amefanya yeye,".DC Muro.