Back to top

Kipengele katika fomu ya chanjo kufanyiwa marekebisho.

29 September 2021
Share

Timu ya wataalam iliyoundwa na serikali kuwahamasisha wananchi wajitokeze kupata chanjo ya Virusi vya Corona imeahidi kukifanyia marekebisho kipengele kilichopo katika fomu inayojazwa na kuisaini kabla kuchanjwa kinachosema serikali haitawajibika kwa lolote kwa mtu anayepata madhara baada ya kupata chanjo hiyo.

Mjumbe wa Tume hiyo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili Prof.Deodatus Kakoko, ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara ya timu hiyo mkoani Kagera.

Prof.Kakoko amesisitiza kuwa chanjo hiyo haina madhara kwa afya ya binadamu kukanusha upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu, ingawa amesema ina kero ndogo ndogo zinazojitokeza kwa baadhi ya watu baada ya kuchanja.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Issessanda Kaniki amesema mkoa huo umeongeza idadi ya vituo vya kutolea chanjo katika kuhakikisha wananchi wanaitumia fursahiyo ya kupata chanjo.