Back to top

Kituo cha michezo cha FIFA kuanza kujengwa Tanga.

15 May 2018
Share


Serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa Kituo kikubwa cha michezo kitachojengwa chini ya ufadhili wa Shirikisho la soka duniani (FIFA) katika eneo la Mnyanjani jijini Tanga ili Tanzania iweze kutumia fursa hiyo kuwekeza katika mchezo wa soka kuanzia ngazi za shule.

Akizungumza mkoani Tanga kuhusu zoezi hilo,Naibu Waziri wa Habari,utamaduni,Sanaa na Michezo Juliana shonza amesema kinachosubiriwa ni fedha kutoka (FIFA) kwa sababu michoro ya kituo hicho tayari imekamilika.

Akifafanua zaidi kwa njia ya simu,Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF) Wallace Karia amesema awali (FIFA) waliwazuia kutokana na kutokidhi matakwa ya kiuhasibu na taratibu za kupata fedha za maendeleo tangu mwaka 2015 lakini hivi sasa wameanza mchakato wa kumaliza tatizo hilo ili waweze kukidhi vigezo.

ITV imetembelea katika eneo la kiwanja ambacho kituo hicho kitajengwa ambapo baadhi ya wakazi waliopo katika eneo hilo wamegoma kuondoka wakidai walipwe fidia hatua ambayo Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya jiji la Tanga ambaye yupo nje ya mkoa kikazi amewataka TFF kama wapo mbioni kuanza wafike ofisini kake ili kuanza mchakato wa kumalizana na wakazi hao.