Back to top

Kiwanda cha uchenjuaji dhahabu cha kwanza nchini kuanza kazi Oktoba.

20 August 2019
Share

Waziri wa madini Mhe.Doto Biteko amesema Tanzania ni miongoni mwa mataifa barani Afrika ambayo yamefikia katika  hatua ya uongezaji dhamani ya madini kufuatia kuanza ujenzi wa kiwanda cha kwanza hapa nchini cha uchenjuaji dhahabu kinachojengwa jijini Dodoma hali itakayosaidia kuwa na mfumo imara wa hifadhi ya taifa ya dhahabu.

Mhe.Biteko ameyasema hayo jijini Dodoma wakati alipotembelea kiwanda cha kwanza cha uchenjuaji madini aina ya dhahabu ambapo amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutawezesha utekelezaji wa sheria inayotaka theluthi moja ya mrahaba unaotokana na madini utolewe kama dhahabu.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge amesema mkoa umejipanga katika kuhakikisha kiwanda hicho kinatoa huduma zake kwa usalama ambapo amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutatoa ajira kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma na maeneo mengine ya jirani.

Naye  afisa mkuu wa uendeshaji wa kiwanda cha kuchenjua madini aina ya dhahabu Bw.Prince Mugisha amesema kiwanda hicho kimekamilika kwa asilimia zaidi ya 70 na mpaka ifikapo October mwaka huu watakuwa tayari wameanza kuchenjua dhahabu kutoka ndani na nje ya nchi.