Back to top

Kongamano la CHADEMA la kudai katiba mpya lagonga mwamba Mwanza.

21 July 2021
Share

Kongamano la Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ) la kudai katiba mpya lililopangwa kufanyika leo jijini Mwanza, kwa mara nyingine tena limegonga mwamba, baada ya viongozi wakuu wa chama hicho kutiwa mbaroni usiku wa manane wakiwa wamelala kwenye hoteli walizofikia.

Taarifa za kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Freeman Mbowe, pamoja na baadhi ya Viongozi wa kamati kuu ya Chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa BAVICHA John Pambalu zilianza kusambaa mapema alfajiri kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

ITV ilifika katika hoteli aliyolala Mbowe na kukuta gari yake aina ya Landcruiser V8 yenye namba za usajili T. 278 AML, ikiwa imeegeshwa nje ya hoteli hiyo, huku mmoja wa walinzi wa hoteli hiyo akidai kuwa kiongozi huyo alikamatwa na askari wenye sare majira ya saa 8 usiku wa kuamkia leo.

Juhudi za ITV kumtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama mkoani humo Mhandisi Robert Gabriel kwa njia ya simu ili kuzungumzia tukio hilo zimegonga mwamba, kufuatia simu zao za viganjani kuita muda wote bila kupokelewa.

Hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia kongamano hilo la katiba mpya kufanyika, limekuja siku moja baada ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel kupiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima.