
Makonteina mawili yaliyokuwa na vitu mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na wataalamu wa kampuni ya utafiti wa gesi na mafuta ya BG kutoka Uingereza, na kuhifadhiwa kwenye Bandari ya Mtwara yamevunjwa na kuibwa vitu vilivyomo ndani, huku watu 6 wakikamatwa kwa tuhuma ya kuhusika na wizi huo.
Kaimu meneja wa bandari ya Mtwara Abilahi Salimu alipoulizwa juu ya kutokea kwa wizi huo kwenye bandari hiyo, alisita kuthibitisha au kukanusha kuhusu tukio hilo, huku akitaka mwandishi wa habari hizi kutokuwa na haraka ya kufuatilia habari hizo.
Hata hivyo, Kamanda wa polisi mkoani Mtwara Kamishna Msaidizi wa polisi Lucas Mkondya amethibitisha kutokea kwa wizi huo ambapo kwenye msako uliofanywa na jeshi hilo wameweza kuwakamata watu 6, kati yao wa nne ni walinzi wa bandari na wawili ni wananchi wa kawaida walioshiriki wizi huo na pia wamelikamata gari aina ya Toyota Mazida yanye usajili Namba T 528 DHW likiwa imebeba viti 66 na mafriji 3 zilizoibiwa toka kwenye makonteina hayo.
Aidha kwenye tukio jingine, Kamanda Lucas Mkondya amesema polisi imewakamata watu wawili walioruka uzio wa kiwanda cha Dangote na kuiba vyuma mbalimbali mali ya kiwanda hicho, na pia wamelikamata gari aina ya Toyota Haice lenye usajiri namba T 945 DMG lililokuwa limebeba vyuma hivyo, na hivyo amewaonya wafanyabiashara wa vyuma chakavu, kuacha kununua vyuma kwa mtu asiyekuwa na hati ya kuthibitisha kuwa ndie mmiliki wa vyuma hivyo, vinginevyo nao watahusishwa katika kushiriki vitendo vya wizi.