Back to top

Kundi la fisi lavamia kijiji laua mtoto Geita.

24 March 2020
Share

Mtoto Nyanjige Hasani mwenye umri wa miaka mitano mkazi wa kijiji cha Nyamigogwa wilayani Nyang'hwale mkoani Geita amefariki dunia baada ya kuvamiwa na  kushambuliwa na kundi la fisi wakati akitoka kutafuta kuni  huku ikidaiwa kuwa ni tukio la nne kwa watoto kufariki  na wameziomba wizara ya maliasili na utalii kuwasaidia kuwadhibiti fisi hao.

Wakizungumza nyumbani kwa wazazi wa marehemu huyo mamia ya wakazi waliofika katika msiba huo wanasema makundi ya fisi yamekuwa tishio kwa binadamu baada ya kushambulia na kuua idadi kubwa ya mifugo na wameiomba serikali kuwasaidia kwadhibiti.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nyamigogwa pamoja na diwani wa kata ya Shabaka wamekiri kutokea kwa matukio ya mauaji ya watoto pamoja na mifugo na wamelifikisha tatizo hilo kwa uongozi wa juu ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Afisa tarafa ya Nyang'hwale  Pira Robert  amewataka wazazi kuchukua hatua ya kuwalinda watoto hasa nyakati za  usiku pamoja na kuwataka wananchi wanaoishi maeneo yenye makundi mengi ya fisi kuondoka ili kuondoa matukio ya kushambuliwa mara kwa mara.