Back to top

Kundi la mbwa laua mtu mmoja na kujeruhi wawili.

19 November 2020
Share

Kundi la mbwa wanaodhaniwa kuwa na kichaa limezua hofu na taharuki wilayani Songea mkoani Ruvuma baada ya kumshambulia mtu mmoja na kumtafuna sehemu  mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake na kujeruhi watu wengine wawili.

Mbwa hao wanaotembea kwa makundi wakiongozwa na kamanda wao aitwae Chui  wanashinda katika makaburi ya Kimolo kabla ya kumuua Bi. Tabita Londo wakamvuta mita nyingi toka nyumbani kwake na kumpeleka jirani na mto Makambi ambako walimtafuna na  kusababisha kifo chake.

ITV imeongea na mmoja wa walioshambuliwa na mbwa hao  Bi. Khadija Ally ambapo hofu imetanda Kata ya Ndilimalitembo na Makambi ambako wanafunzi wa awali wameshindwa kwenda shule kwa siku moja kwa hofu ya kushambuliwa na mbwa hao.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma  ACP Simon Maigwa Marwa akizungumza kwa simu na ITV amesema anaendesha operesheni kwa kushirikiana na idara ya mifugo kuwasaka mbwa hao ambapo tayari wameshawaua mbwa kumi huku wananchi wakiwaua mbwa nane.

Akizungumza kwa simu kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea Bw. Pololet Mgema amewataka wananchi waliofuga mbwa kuwafungia mbwa wao na pia kujiridhisha kama mbwa wao hawana kichaa cha mbwa.