
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio la usitishaji mapigano mara moja Gaza, siku chache baada ya Marekani kutumia kura ya turufu kuzuwia azimio kama hilo katika Baraza la Usalama.
Mataifa ya Kiarabu na yenye idadi kubwa ya Waislamu yalikuwa yameitisha kikao cha dharura cha Baraza hilo lenye nchi 193 wanachama kwa ajili ya kura hiyo iliyopigwa usiku wa kuamkia Jumatano Disemba 13.
Nchi 153 zimeliunga mkono azimio hilo, huku 10 tu zikilipinga.
Miongoni mwa nchi 10 zilizopiga kura ya hapana ni Marekani na Israel, zikiungwa mkono na Czechia, Austria, Guatemala, Liberia, Micronesia, Nauru, Papua New Guinea, na Paraguay.
