Lissu kuondoa utitiri wa Kodi kwa wachimbaji wadogo.

Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CHADEMA Mhe.Tundu Lissu amesema iwapo atachaguliwa kuongoza serikali ya awamu ya sita katika uchaguzi mkuu ujao, ataondoa utitiri wa kodi kwa wachimbaji wadogo na badala yake kodi zote zitalipwa na wanunuzi wakubwa wa madini.

Akiomba kura kwa wananchi wa Kakola jimbo la Msalala baada ya kumsimamisha njiani akitokea mjini Kahama kuelekea Mbogwe, Bukombe na Chato kuendelea na mikutano ya kampeni zake, mgombea Urais huyo wa Tanzania Mhe.Tundu Lissu pia amewaomba watu walio na vitambulisho vya wajasiriamali kuvitunza ili serikali ya CHADEMA ikiingia madarakani waweze kurejeshewa fedha zao.

Akinadi ilani ya chama chake kilichompa ridhaa ya kuingia katika kinyang'anyiro cha Urais wa Tanzania, katika uwanja wa shule ya msingi masumbwe wilayani Mbigwe na Ushirombo - Bukombe, Mhe.Tundu Lissu halikadhalika ameahidi neema kwa wafugaji kwa kuwahaidi kuwatafutia malisho kwenye mapori ya akiba, ili kuondoa changamoto ya kukamatiwa mifugo yao.

Kampeni za Tundu Lissu za kuchanga karata ili kupata turufu itakayomwezesha kuingia ikulu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa siku ya leo zimehitimishwa wilayani Chato, ambako amewaomba wananchi wenye sifa za kupiga ura kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 28 ili kuchagua viongozi wanaotokana na CHADEMA ambao watasimamia maendeleo ya watu .