
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt.Angeline Mabula, amewataka maafisa wa sekta ya ardhi nchini kuwafuata na kuwahudumia wananchi, katika mitaa yao ili kutoa huduma za ardhi kwa ufanisi.
Waziri Mabula ameyasema hayo wakati alipofanya ziara, katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma zinazotoa huduma za ardhi kwa wananchi ambapo alikuta msongamano mkubwa usiofuata utaratibu unaosababisha kero nyingi kutoka kwa wananchi ambao walimfikishia kero hizo.
Dkt.Mabula amewataka maafisa wanaohudumia wananchi kuongeza muda wa kazi kuanzia saa 2 kamili asubuhi hadi saa 12 kamili jioni badala ya muda wa awali ambao walikuwa wanamaliza saa tisa alasiri jambo ambalo wananchi wengi wamelilalamikia na kuomba kuwe na utaratibu mzuri wa utowaji huduma bila upendeleo.
Aidha, Waziri Mabula amekemea tabia inayofanywa na maafisa wa sekta ya ardhi ya umilikishaji wa kiwanja kimoja kwa watu wawili au zaidi unaojulikana kama Double Allocation ambao kwa jiji la Dodoma unaonekana kushamiri na kusababisha malalamiko na migogoro mingi ya ardhi.
Dkt. Mabula ametumia fursa hii kuwafahamisha wananchi kuwa kwa sasa Wizara yake ipo katika kuboresha mfumo wa taarifa za ardhi kwa kutoa huduma kwa njia ya mtandao wa simu ambapo wananchi watafanya miamala ya huduma za sekta ya ardhi kupitia simu zao.