
Kampuni ya Sukari Kilombero, ambayo ni mzalishaji mkubwa wa sukari nchini, imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuboresha maisha ya jamii, kwa kuunga mkono miradi mitatu ya maendeleo iliyoanzishwa na jamii katika Bonde la Kilombero.
Kampuni ya sukari Kilombero imechangia ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Nyamvisi, Maabara ya Zahanati ya Kijiji cha Ruaha, pamoja na Eneo la Kusubiria Wagonjwa katika Kituo cha Afya Kidodi. Ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo, Kilombero Sugar imekabidhi mifuko 300 ya saruji, nondo 300 za ukubwa wa milimita 12, pamoja na miche 150 ya miti, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya miundombinu sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Mchango huu umetolewa kupitia mkakati wa kampuni wa uundaji wa thamani ya pamoja unaolenga kuhakikisha ukuaji wa biashara unaenda sambamba na maendeleo ya jamii. Badala ya kuanzisha miradi mipya, Kilombero Sugar imeamua kushirikiana na jamii katika kukamilisha miradi ambayo tayari imebuniwa na kuanzishwa na wananchi wenyewe, jambo linaloonesha dhamira ya pamoja ya kuleta maendeleo jumuishi na endelevu.
Akizungumzia mpango huo, Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano kwa wadau kutoka Kilombero Sugar, Bw. Victor Byemelwa, amesema mchakato wa kuchagua miradi ya kunufaika ulizingatia tathmini ya kina ya mahitaji ya jamii, ikiwemo umuhimu wa mradi kwa wananchi, utayari wa jamii kuutekeleza, pamoja na uwepo wa mpango madhubuti wa utekelezaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Kilombero Sugar, Bw. Derick Stanley, alisema kampuni itaendelea kuwekeza katika miradi inayozalisha manufaa ya kudumu kwa jamii zinazozunguka shughuli zake.
"Tunaamini mafanikio ya Kilombero Sugar hayawezi kutenganishwa na ustawi wa jamii zinazotuzunguka. Kupitia mkakati wetu wa Creating Shared Value, tunawekeza katika miradi inayojibu mahitaji halisi ya wananchi huku ikizalisha thamani ya muda mrefu kwa jamii na uchumi. Mchango tunaoutoa leo unaonesha dhamira yetu ya kuimarisha huduma za jamii, kuwawezesha wananchi na kujenga ushirikiano imara unaochochea maendeleo endelevu ya Tanzania."
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa na Mgeni Rasmi, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, ameipongeza Kilombero Sugar kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi.
"Kilombero Sugar imeendelea kuonesha kuwa uwajibikaji wa kampuni hauishii katika shughuli za biashara pekee. Mchango huu utaboresha huduma za afya, kuimarisha utawala wa vijiji na kuongeza ustawi wa wananchi. Tunapongeza kampuni kwa kushirikiana na Serikali katika kuharakisha maendeleo endelevu na tunatoa wito kwa taasisi nyingine za sekta binafsi kuiga mfano huu."
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamvisi, Bw. Yohana Kibasa, ameishukuru Kilombero Sugar kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii na kuwataka wadau wengine kuendelea kushirikiana na jamii katika kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi.
Naye Dkt. Siriana Madumla, akiwakilisha wanufaika wa mradi wa eneo la kusubiria wagonjwa katika Kituo cha Afya Kidodi, amesema vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuharakisha ujenzi wa jengo hilo na kuboresha huduma kwa wananchi wengi wanaotegemea kituo hicho.
Aidha, utoaji wa miche 150 ya miti unaonesha dhamira ya Kilombero Sugar katika kuendeleza uhifadhi wa mazingira na kujenga jamii zenye mazingira safi na endelevu.
Ikiwa ni miongoni mwa kampuni zinazoongoza katika sekta ya kilimo-biashara nchini, Kilombero Sugar itaendelea kushirikiana na Serikali, jamii na wadau mbalimbali katika kuanzisha na kuunga mkono miradi yenye kuleta maendeleo endelevu, kuimarisha taasisi za jamii na kujenga thamani ya pamoja kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
