Back to top

"MAAFISA UGANI BADILINI MFUMO WA UFUGAJI"DC KANONI

21 March 2024
Share

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe.Lauter Kanoni, amewasisitiza maafisa ugani kuhakikisha wanabadili mfumo wa ufugaji kutoka ule wa holela hadi ufugaji wa kisasa.

Mhe.Kanoni amewataka watalaam hao katika sekta ya Mifugo kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo kwa mifugo ili kuepusha madhara kwa mifugo na watumiaji wa mazao ya Mifugo hiyo.

Amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imeendelea na zoezi la kuwanoa maafisa ugani wa sekta ya Mifugo waliopo Kanda ya Kusini, inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye mafunzo yaliyofanyika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzake, Daktari wa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bi.Subira Simbeye, ameahidi kwenda kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Kanoni ili kuendelea kuboresha sekta ya Mifugo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Awali akiwasilisha mada ya "Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma", Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Wizarani hapo Bi. Suzan Silayo amewataka Maafisa ugani hao Kufanya kazi kwa uadilifu, kuzingatia maadili ya utumishi na kufuata sheria kanuni na taratibu za kiutumishi.

Aidha Bi.Silayo amewataka wataalam hao kuepuka kutoa au kupokea rushwa huku pia akiwasisitiza kujiandaa na maisha ya baada ya kustaafu katika Utumishi wa Umma kwa kuhakikisha wanafanya uwezekaji wa kutosha pindi wakiwa kazini.

Mafunzo hayo kwa Maafisa Ugani wa mikoa ya kanda ya Kusini yatafanyika kwa siku 2 ambapo mada mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa kwa wataalam hao kwa lengo la kuwakumbuka taratibu mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yao pindi wakiwa uwandani.