Back to top

MAAFISA UGANI NDIO INJINI YA NCHI KUWA KAPU LA CHAKULA BARANI AFRIKA

20 November 2023
Share


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa Ugani kutumia taaluma zao vizuri, ili kusaidia kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya sita, inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinazalisha vya kutosha na kuiwezesha nchi kuwa kapu la Chakula Barani Afrika.

Prof. Shemdoe amesema hayo wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Ugani nchini (TSAEE) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega unaofanyika Jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa Sekta hizo Serikali imekuwa ikiongeza bajeti kila mwaka lengo likiwa kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo kwa kuongeza tija kwenye uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na lishe; Kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na kuongeza mauzo ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi.

Aliendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi ambao wanaonesha dhamira ya dhati ya kuungana na serikali katika kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati kupitia shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi. 

Aidha, aliwataka Maafisa Ugani hao kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwenye mradi wa kielelezo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT).

"Nyinyi ndio washauri wa kwanza katika programu ya BBT ambayo imelenga kuwainua vijana, utaalamu wenu utasaidia kutimiza malengo ya Rais, Dkt. Samia ya kuwainua vijana na kina mama hapa nchini", alibainisha 

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Ugani(TSAEE), Prof. Catherine Msuya alizishukuru Wizara za kisekta kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa Ugani huku akiomba Wizara hizo ziendelea kukilea chama hicho kwa kukitengea  bajeti ili chama hicho kiweze kujiendesha bila matatizo.

Halikadhalika, aliziomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kilimo na TAMISEMI kuboresha na kuweka mfumo mmoja ambapo utawawezeaha Maafisa Ugani hao kuwasiliana vyema tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna mifumo mingi tofautitofauti.