Back to top

MAAMBUKIZI YA MALARIA YAPUNGUA KWA ASILIMIA 6.7 NCHINI

12 May 2025
Share

Tafiti za viashiria vya ugonjwa wa Malaria nchini zinaonesha umepungua kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022 ikiwa ni hatua kubwa zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Mei 12, 2025 wakati akizindua awamu ya pili ya ugawaji wa dawa za kuua viuadudu vinavyosababisha uwepo wa mbu wanaozalisha ugonjwa wa Malaria nchini, katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Peramiho.

Amesema, bado mikoa mengine maambukizi yapo juu ikiwemo mkoa wa Tabora 20%, Kagera 18%, Shinyanga 16%, lakini kuna mikoa ambayo maambukizi ni chini ya asilimia 1 ikiwemo mikoa ya Arusha, Manyara, Dar es Salaam, Songwe, Mwanza, Iringa pamoja na Singida

“Vifo vinavyotokana na Malaria vimepungua kutoka vifo 6,311 kwa mwaka 2015 hadi kufikia vifo 1,503 kwa mwaka 2024, tunamshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake,” amesema Waziri Mhagama.

“Leo tumezindua awamu hii ya pili ya kugawa dawa za viuadudu vinavyosababisha uwepo wa ugonjwa wa Malaria ambazo zitatumiwa na halmashauri zote nchini kwa kuwa ni lazima sasa hivi tujikite katika kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria ambao ni kati ya magonjwa yanayosababisha vifo nchini,” amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga Shilingi Bilioni 10 ili kununua lita 833,333 ambazo ni dawa za viuadudu vya Malaria zinazozalishwa nchini (Kibaha, Pwani) ambazo zitasambazwa katika halmashauri zote ili kukomesha uwepo wa Mbu hao.

“Awamu ya kwanza dawa hizi tulizigawa katika halmashauri 57, Mhe. Rais ameiagiza Wizara ya Afya kuendelea kugawa dawa hizo katika halmashauri 127 zilizobakia ikiwemo Halmashauri yetu ya Wilaya ya Songea, tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za Watanzania,” amesema Waziri Mhagama.