Back to top

Mabasi ya abiria yaendayo mikoani kuhamia stendi ya Nyabulogoya Mwanza

25 August 2019
Share

Wafanyabiashara wa soko kuu la Mwanza pamoja na wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani waliopo stendi ya Nyegezi jijini Mwanza, wameagizwa kupisha na kuelekea kwenye maeneo ya muda waliyopangiwa kabla ya Septemba 5 mwaka huu ili kuruhusu ujenzi wa soko kuu jipya pamoja na stendi ya mabasi ya kisasa kujengwa.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi wakati alipoongoza timu ya viongozi na watendaji wa halmashauri ya jiji hilo kumuonyesha mkandarasi mzawa kampuni ya Mohammed Builders ya jijini Dar es Salaam mipaka ya ujenzi na michoro ya stendi mpya na ya kisasa pamoja na soko kuu jipya la mkoa wa Mwanza ambayo kwa pamoja itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 38.

Mabasi yaendayo mikoani yaliyokuwa stendi ya Nyegezi kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, yatahamia kwenye stendi ya muda ya Nyabulogoya kata ya Nyegezi iliyopo umbali wa kilometa moja kutoka stendi ya zamani, huku wafanyabiashara wa soko kuu wakitakiwa kuhamia kwa muda kwenye soko la Mbugani kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita ambao miradi hiyo itakuwa imekamilika

Mbunge wa jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula amewaomba wafanyabiashara waliopo soko kuu la Mwanza pamoja na wamiliki wa mabasi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo ili ujenzi wa miradi hiyo miwili mikubwa katika jiji la Mwanza ianze mara moja.