
Waziri wa Ujenzi Mh.Innocent Bashungwa amesema, serikali inakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa madaraja makubwa mawili ya Kalebe katika barabara ya Kyaka – Katoro – Kyetema na Daraja la Kyanyabasa katika Mto Ngono, ili kukidhi mahitaji ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Bukoba Vijijini.
Bashungwa ameyasema hayo, wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Katoma Wilaya ya Bukoba Vijijini, katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, mkoani Kagera.

Bashungwa ameeleza kuwa katika eneo la Kyanyabasa litakapojegwa daraja, Wananchi walikuwa wanapata huduma ya usafiri kwa Kivuko cha TEMESA ambacho kilikuwa kinatoa huduma kwa kusua sua na kupelekea Serikali kufanya maamuzi ya kujenga daraja kubwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Kyaka – Katoro –Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.7 kwa kiwango cha lami kwa kuanza na kipande cha kilometa 10 kitakachojengwa sambamba na ujenzi wa Daraja la Kalebe na kueleza kuwa Makandarasi atafika eneo la mradi kufika mwezi Disemba, 2024.
