
Jeshi la Polisi nchini limesema litawafungia leseni madereva wote wanaosababisha ajali na kubainisha kuwa katika siku za hivi karibuni kumeendelea kujitokeza ajali za barabarani zilizosababisha vifo na majeruhi kwa watanzania.
Msemaji wa jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP, David Misime, amebainisha kuwa uchunguzi unapofanyika zinaonyesha chanzo ni uzembe wa madereva wanaoendesha magari hayo.
Misime amesema chanzo cha ajali hizo ni uzembe pamoja na mwendo kasi na kupita magari mengine (Overtake) bila kuchukua tahadhari maeneo ambayo alama za barabarani zimekataza.
Amesema kuwa pamoja na uzembe huo unaofanywa na baadhi ya madereva wa magari hayo kumekuwa na maneno ya kuiaminisha jamii kuwa mwisho wa mwaka ajali zinakuwa nyingi, jambo ambalo si sahihi huku akiwataka madereva kuondoa dhana hiyo ambayo inapotosha umma wa Tanzania.
SACP Misime amebainisha kuwa kufika kwa mwisho wa mwaka hakujabadili sheria za usalama barabarani wala alama za makatazo na ishara za barabarani ambapo amewataka madereva kuzifuata sheria hizo ili kuepuka ajali za barabarani.