Back to top

Maduka yafungwa kwa saa kadha mtwara kwa kuhofia maandamano.

26 April 2018
Share

Maduka mengi na soko kuu katika mji wa Mtwara yamechelewa kufunguliwa kwa saa kadhaa, kwa hofu ya kufanyika kwa maandamano, huku wananchi wanaotafuta mahitaji wakilalamikia kukosa huduma wanazozitafuta na hivyo kuiomba serikali kusaidia kuhakikisha huduma zinarejeshwa kama kawaida.

ITV ilifika kwenye soko kuu Mtwara na kukuta maduka yakiwa yamefungwa ambapo wananchi wengi waliokuja soko kuu walijikuta wakilazimika kurudi majumbani bila kupata mahitaji. 

Hata hivyo ITV ilikutana na mmoja wa wafanyabiashara wa duka Ibrahimu Kaseka aliyefungua biashara yake, alipoulizwa alieleza ameamua kufungua biashara yake bila hofu yoyote, kwa kuamini yupo salama kutokana na kuwepo kwa doria na uwezo wa jeshi la polisi la kulinda usalama wao na mali zao. 

Uchunguzi wa ITV umeonyesha huduma zingine kama daladala na boda boda na biashara kwenye soko la mbogamboga eneo la sabasaba zimekuwa zikiendelea kama kawaida ambapo baadhi ya wananchi wamesema wanachojua ni siku ya maadhimisho ya siku tukufu ya muungano na sio maandamano, hata hivyo baadhi ya mabasi yanayosafiri kwenda wilayani na mkoa jirani wa lindi wamelalamikia, hofu ya kuwepo kwa maandamano imeathiri kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa abiria, kutokana na idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kusafiri. 

Kamanda wa polisi mkoani Mtwara Kamishina msaidizi wa polisi Lucas Mkondya amesema hali ya usalama mkoani humo imeimarishwa, lakini akabainisha kabla ya leo polisi imewafikisha mahakamani wanafunzi wa 2 wa chuo kikuu cha sauti tawi la mtwara kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano kwenye mitandao, na wanafunzi wengine 7 wanahojiwa kuhusiana na tuhuma hizo hizo.