
Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani hapa nchini yanahitaji ushirikiano baina ya sekta binafsi, na wadau wa maendeleo ili kuleta matumaini kwa wale ambao watakuwa wamepata changamoto ya maradhi ya hayo.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika jukwaa la uwekezaji linalolenga kuimarisha huduma za saratani nchini, ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, watafiti na wataalamu wa tiba kunaweza kubadilisha taswira za huduma za matibabu ya saratani nchini.
RaisDk.Mwinyi amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani kwa kujenga miundombinu ya huduma za afya, mikakati ya upatikanaji wa huduma bora za matibabu bora kwa wote.
Kadhalika Rais Mwinyi ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutambua umuhimu wa ushirikiano ili kufikia malengo kwa kuwekeza rasilimali fedha katika kuimarisha utafiti, kuboresha miundombinu ya afya, na kuhakikisha upatikanaji matibabu sawa kwa wagonjwa wa saratani nchini na kuishukuru Serikali ya Marekani kwa ushirikiano wao kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya nchini.
