Back to top

Magufuli:Vijiji na vitongoji vilivyopo maeneo ya hifadhi visiondolewe.

15 January 2019
Share

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kusitishwa mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana viongozi mbalimbali akiwemo na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.

Pamoja na agizo hilo Mhe.Rais Magufuli ametaka viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima ambao kwa sasa wanataabika kupata maeneo ya kufugia wanyama na kuzalisha mazao.

Mhe.Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya zoezi la uwekaji wa mipaka ya hifadhi na makazi,na kutumia busara katika uwekaji wa mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kuwaondoa.